Email: info@jkuz.go.tz | P.o.Box: 985 | Tel: 0242238030 | Fax: 0242232149
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi(JKU) Kanal Makame Abdalla Daima aliwataka watendaji wa JKU kutekeleza Maazimio ya Mpangokazi ya mwaka 2023 ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Wito huo aliutoa wakati alipokua akifunga mkutano mkuu wa JKU wa kutathmini Malengo ya miradi ya maendeleo uliofanyika ukumbi wa Makao Makuu ya JKU Saateni.
Alisema jukumu kubwa la JKU ni kuongeza uzalishaji kupitia makambi mbali mbali sambamba na kuimarisha malezi ya vijana wa kujitolea ambao hupata mafunzo ya Ujasiriamali na Uzalendo.
“Tutahakikisha tunakuza miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha kilimo na ufugaji kwa maslahi ya JKU na Taifa kwa Ujumla” alisema Kanali Daima.
Akiwasilisha mada Mkuu wa Idara ya Uchumi na uzalishaji mali Kanali Jabir Saleh Simba alisema kuwa dhamira ya JKU ni kuboresha kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Ufundi sambamba na kuanzisha kampuni ya kudumu ya ujenzi ambayo itasaidia kukuza kipato ndani ya JKU.
Hata hivyo Kanali Jabir alisema kuwa JKU pia ina mpango wa kuongeza wataalamu katika miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Utawala wa JKU Luteni Kanali Haji Ali Ali alisema atahakikisha anasimamia ipasavyo majukumu ya watendaji wake ili waweze kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.
Mkutano huo wa siku tatu ulijumuisha Wakuu wa Zoni, Wakuu wa Kambi, Idara pamoja na Vituo vya Uzalishaji mali ndani ya JKU.